Tuesday, August 26, 2014

ANGALIA PICHA-HALI INATISHA KITUO CHA WALEMAVU CHA BUHANGIJA MJINI SHINYANGA

Hapa ni katika kituo cha kulea watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali cha Buhangija katika manispaa ya Shinyanga na hiki ni chumba cha wavulana, ambapo wamelazimika kuanza kulala kwenye jengo hilo kabla halijakamilika likiwa halina milango wala madirisha kutokana na kuwepo msongamano mkubwa wa watoto na kusababisha kulala kitanda kimoja watatu hadi wanne kutokana msongamano uliopo, ambao umesababishwa na kuwepo mauaji ya watu wenye albinizim hapa nchini hususani mikoa ya kanda ya ziwa na magharibi hivyo kituo hicho kutumika kulea walemavu hao wakiwemo wasioona,wasiosikia na Albino ambao ndiyo idadi kubwa wakitoka mikoa ya Simiyu,Geita,Mwanza,Tabora na Shinyanga.
Meya wa manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi misaada iliyotolewa na wadau kupitia shirika la Easy flex production la mjini Shinyanga,ambao walitoa chakula,mashuka na fimbo nyeupe za walemavu wasioona.
Mkurugenzi mtendaji wa Easy Flex Production Happiness Kihama akisoma taarifa ya misaada waliyoitoa kwenye kituo hicho, kupitia harambee waliyoitisha ya kuchangia kituo cha Buhangija na kambi ya wazee Kolandoto vyote vya manispaa ya Shinyanga ambapo msaada uliotolewa una thamani ya sh milion 7,840,000.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Buhangija na msimamizi wa kituo hicho Peter Ajali akitoa maelezo kwa Meya wa manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam juu ya changamoto zilizopo ,alisema kwa sasa watoto wanalazimika kulala wanne kitanda kimoja kutokana na idadi kubwa ya watoto hasa Albino kufuatia kuanza kuibuka tena mauaji hayo mkoa wa Simiyu na Tabora wawili kujeruhiwa kwa kukatwa viungo vyao vya mwili.
Hili ni bweni la wasichana ambao hulala wanne kitanda kimoja hivyo kuwa na msongamano mkubwa licha ya wadau mbalimbali kusaidia kutoa misaada lakini bado haijakidhi mahitaji .
Meya akimkabidhi msimamizi wa kituo hicho mwalimu Peter Ajali, fimbo nyeupe 11 za watoto wasioona.
Mkama Shakengwa akiweka wazi mauaji ya albino yanavyotishia amani ya nchi kutoweka na kusababisha waishi kama wakimbizi nchini kwao na kuitaka serikali kutoa adhabu kali kwa wanaobainika kufanya unyama huo.

Mwenyekiti wa kamati inayosimamia upatikanaji wa misaada hiyo DKT.Ntoke akionyesha fimbo nyeupe zilizotolewa na Easy flex Production kwa ajili ya watoto wasioona.
Meya akikagua kisima cha maji cha kupampu kwa mkono akiwa na viongozi wa Easy flex .
Baadhi ya watoto wenye albinizim wanaosoma darasa la saba shule ya Buhangija Rehema Masunga na Dorcas Sonda wakiishukuru Easy flex kwa msaada walioutoa .
Baadhi ya vyakula vilivyotolewa na wadau
WATOTO wenye ulemavu  wa ngozi  katika kituo maalumu cha kulea  watoto hao Buhangija manispaa ya Shinyanga ,wamezidi kuongezeka kituoni hapo  kutokana na wimbi la mauaji y a albino  kuibuka tena na kufikia watoto zaidi ya  100  kupelekwa hapo kutoka maeneo mbalimbali kwa hofu ya kuuwawa na kufanyiwa  ukatili.

Imeelezwa kuwa watoto wengi wametoka kwenye  mikoa ya Tabora,Simiyu na Mwanza ikiwa  watoto wa kike  98 na  wakiume 96 , baada ya mauaji hayo kuibuka  tena tangu kwenye  mwezi mei mwaka huu kwa kuuawa mwanamke mmoja huko mkoani Simiyu na mkoani Tabora  watu wawili  kuuawa kwa kipindi kifupi,ambapo  kila siku watoto watatu mpaka wanne wanaletwa kituoni hapo. 

Hayo yameelezwa na watoto hao mwishoni mwa wiki iliyopita kwa waandishi wa habari kituoni hapo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi misaada iliyotolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo, kupitia harambee iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali Easy flex la mjini Shinyanga kwa ajili ya kusaidia watoto hao .

Baadhi ya watoto wa kituo hicho  wanaosoma shule ya msingi Buhangija darasa la saba Rehema Masunga,Mkama Shakengwa walisema nchi ya Tanzania inasifika kwa kuwa na amani lakini sasa hali inaelekea kuwa mbaya kutokana na baadhi ya watu kuwa na roho za kikatili na kuua watu wasiokuwa na hatia

“Inasikitisha sana kuibuka tena mauaji ya albino tuliona kwenye vyombo vya habari watu wamekatwa mkono,naiomba jamii iwapuuze waganga wa kienyeji maana ndiyo wanachangia, tumuamini mungu atatuepusha na unyama huu wa kikatili”alisema Daniel Limbu.

Naye mwalimu mkuu wa shule hiyo ambaye pia ni msimamizi wa kituo hicho Peter Ajali,alisema kufuatia kutokea kwa matukio mawili ya albino kukatwa viungo vyao vya mwili mkoani Tabora na mmoja Bariadi kuuawa  matukio hayo yamesababisha kuongezeka idadi ya watoto kituoni hapo hivyo kuwa na msongamano mkubwa.

Akizunguma kwenye hafla hiyo meya wa manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam aliitaka jamii kuwa na utamaduni wa kusaidia kituo hicho,badala ya kutegemea msaada kutoka kwa wafadhili huku akisisitiza mikoa yote iliyopeleka watoto kutoa michango itakayosaidia kukidhi mahitaji na kuwaomba kuielimisha jamii umuhimu wa kusaidia.

Awali mkurugenzi mtendaji wa Easy flex production Happness Kihama alisema changamoto kubwa iliyopo ni uelewa mdogo kwa jamii ,juu ya kusaidia vituo hivyo vyenye mahitaji maalumu wazee na walemavu kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali ,ikiwa ni pamoja na uchakavu wa majengo,chakula na malazi.


PICHA NA HABARI KWA HISANI YA STELLA BLOG NA KARENY BLOG
My Blogger Tricks
blogger

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2014 KAYANDA All Right Reserved
Designed by MALUNDE.