Tuesday, July 7, 2015

Wazee kata ya Nyihogo wilayani Kahama wasikitishwa na mrundikano wa vilabu vyapombe

Diwani wa Kata ya Nyihogo Amos Sipemba


WANANCHI wa kata ya Nyihogo Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wametoa malalamiko yao mbele ya Diwani wa kata hiyo anayemaliza muda wake wakisikitishwa na kata hiyo kuwa na vilabu vingi vya Pombe za Kienyeji na kufanya biashara  hiyo usiku kucha  katika nyumba za kuishi hali itakayofanya kuwa na Taifa la walevi.

Katika kikao hicho kilichoandaliwa na Diwani wa Kata hiyo Amos Sipemba (CHADEMA) kwa nia ya kuongea na wazee wa kata hiyo na kuwaomba ridhaa ya kuomba Udiwani kwa kipindi kingine, Wazee hao wamesema kuwa Madiwani wengi inapofika nyakati za mwisho za uongozi wao ndio wanapata fursa ya kuwakumbuka wazee.

Wamesema kuwa Vilabu hivyo vya Pombe vimekuwa vikifanya kazi bila ya kufuata maelekezo ya vibali vyao na hivyo kuleta kelele nyingi nyakati za usiku kwa kuwa vilabu hivyo vipo karibu zaidi na Makazi ya watu na kwamba navyo vimegeuka kuwa Night Club za mitaani.

Mmoja wa Wazee hao Khamis Mluya almesema Vilabu hivyo pia vimekuwa vikifuga majambazi na wakabaji kwa kuwa vinakesha hali ambayo inasababisha ikifika majira ya saa tisa za usiku Vijana wanaokunywa humo huamka na kufanya shughuli za ukabaji hali ambayo inatia wasiwasi katika kata hiyo na kusema Diwani huyo ameshindwa kuidhibiti hali hiyo.

Mluya aliendelea kusema kuwa pamoja na mambo mengine kata hiyo pia imekuwa na mrundikanyo wa watoto ambao hawasomi shule wa kuanzia umri wa miaka nane hadi kumi na mbili wanajishughulisha na biashara ya kuokota vyuma chakavu na kuenda kuviuza kwa lengo la kupata fedha.

“Nakuambia Mheshimiwa Diwani wa kata ya nyihogo tatizo hili ni kubwa la wingi wa watoto na tusipoangalia tunaweza kuunda Taifa la walevi na wabeba vyumba chakavu msitegemee hapo baadaye kutakuwa na wasomi”, Alisema Mzee Khamis Mluya.
Wazee wa Nyihogo wakimsikiliza Diwani wao
 Wazee hao waliitaka Serikali kuhakikisha kuwa inatumia meno yake katika kuhakikisha watoto hawa wanarudi makwao na kuondelea na masomo na kuongeza kuwa kama viongozi hao watakaa kimya basi kuna uwezekano wa kundi hilo kuwa Waporaji nam majambazi wa siku za baadaye.

“Watoto hawa utashangaa ukiacha Sufuria nje ya nyumba ni mali yao, wakikuta Vijiko ni mali yao, sasa Mweshimiwa tutegemee nini kwa kundi hili ambazlo kwa sasa limekuwa kero katika kata ya Nyihogo tunaomba msaada wenu wa haraka”, Aliongeza Mluya.

Kwa upande wake Afisa mtendaji wa mtaa wa Nyihogo na Sazia katika kata ya Nyihogo Simon Mabumba amewaomba Wazee na Wananchi wa kata hiyo kushirikiana katika kuondoa matatizo hayo kwani wanaofanya mambo hayo ni watoto wao wanaoishi nao majumbani hali ambyo inakuwa ngumu katika kuwakamata.

Afisa mtendaji wa mtaa wa Nyihogo Simon Mabumba
Pia Mtendaji  huyo ameshauri Serikali kurudisha Vipindi vya Dini Mashuleni ili Wanafunzi waweze kufundishwa maadili na Nidhamu kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma hali ambayo inaweza kuchangia katika kupunguza wimbi la watoto hao.

Na Paul Kayanda Kahama
My Blogger Tricks
blogger

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2014 KAYANDA All Right Reserved
Designed by MALUNDE.